Friday 14 June 2013

MAKALA KUSU USIKU WA TUZO ZA 'KTMA 2013 - KIKWETU KWETU'



Mshindi wa tuzo tatu za Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2013, Kala Jeremiah (katikati) akitoa neno la shukrani. Kushoto ni Mtayarishaji D Classic aliyefanya wimbo Dear God uliompa Jeremiah tuzo hizo.

Mwanamuzi Hussein Jumbe, akichana mistari ya kibao cha Khaleed Mohammed 'TID' kiitwacho Zeze katika usiku huo ndani ya Ukumbi wa Mlimani City.

Mkongwe Zahir Ali Zorro akikitendea haki kibao cha mkali wa Takeu, Lucas Mkenda kiitwacho Kikulacho.

Ommy Dimpoz kulia akipokea kutoka kwa msanii wa filamu nchini Wema Sepetu, tuzo ya Wimbo Bora wa Kushikiana uitwao Me and You aliomshirikisha Vanessa Mdee (katikati).
DAR ES SALAAM, Tanzania
KI-KWETU Kwetu ilikuwa ndio kaulimbiu iliyobeba mchakato wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (Kilimanjaro Tanzania Music Awards – KTMA 2013), zilizofikia tamati Juni 8, katika Usiku wa Tuzo hizo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hali ya mambo ilikuwa ya kuvutia mno katika usiku ule uliotanguliwa na kimya cha dakika moja kuomboleza kifo cha Albert Mangweha ‘Ngwea’ aliyefariki Mei 28 nchini Afrika Kusini na kuzikwa Juni 6, katika makaburi ya Kanisa la Mtakatifu Monica, Kihonda mjini Morogoro.
Burudani kali iliupamba usiku ule, huku mambo yakinoga kila dakika zilivyokuwa zikiyoyoma; kabla, wakati na hata baada ya tuzo hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager ‘Bonge la Kiburudisho.’
Waliohudhuria ‘Usiku wa Tuzo’ Mlimani City Jumamosi ile, watakuwa mashahidi wa hili na kwa kutambua thamani ya kilichofanywa na waratibu na wadhamini wakuu Kilimanjaro, nathubutu kusema; Hongera TBL, lakini pia kwa Basata na Innovex kwa kufanikisha mchakato.
Hongera kwa kufanikisha mchakato mzima wa KTMA 2013, ulioambatana na tuzo mili za ‘All of Fame’ iliyoenda kwa Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje na ile ya ‘Individual All of Fame’ iliyoenda kwa nyota wa zamani wa bendi ya Cuban Marimba, marehemu Salum Abdallah.
Hapa tunakuletea kwa ufupi matukio muhimu katika ‘Usiku wa Tuzo,’ ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa aina yake kwa wasanii Kala Jeremiah, Ommy Dimpoz na Chalz Baba na Bendi yake ya Mashujaa kwa kutwaa tuzo nyingi kati ya tuzo 37 zilizotolewa.
Kala Jeremiah, Dimpoz, Mashujaa wang’ara KTMA

Kama ni utabiri uliotimia, gazeti hili linaweza kujivunia kuwatabiria vema wasanii Kala Jeremiah na Ommy Dimpoz, ambao kupitia moja ya makala zake iliwataja kuwa ni wasanii walio kwenye nafasi nzuri ya kuibuka na tuzo nyingi na kujiwekea rekodi. Usiku wa Tuzo KTMA 2013 ukathibitisha hilo kwa wakali hao kushinda tuzo tatu kila mmoja.

Kala Jeremiah alikuwa na usiku wa aina yake, ambapo alikuwa karibu atwae tuzo nne, ingawa aliishia kutwaa tatu za Wimbo Bora wa Mwaka (Dear God), Msanii Bora wa Hip Hop na ile ya Mtunzi Bora wa Hip Hop, huku akiipoteza ile ya Wimbo Bora wa Mwaka wa Hip Hop (Dear God) iliyoenda kwa Nay wa Mitego kupitia wimbo Nasema Nao.

Kwa upande wa Dimpoz, nyota pekee aliyekuwa akiwania tuzo nyingi zaidi (saba) katika kinyang’anyiro hicho, alipata tuzo tatu za Wimbo Bora wa Bongo Pop (Me and You aliomshirikisha Vanessa Mdee), kibao kilichompa pia tuzo ya Wimbo Bora wa Ushirikiano.

Dimpoz akapokea tuzo ya tatu ya Video Bora ya Mwaka kupitia kibao cha Baadae, huku akichemka katika kategori nne za Wimbo Bora wa Mwaka, Msanii Bora wa Mwaka wa Kiume, Msanii Bora wa Mwaka wa Kiume wa Bongo Flava na Mtunzi Bora wa Mashairi wa Bongo Flava.

Bendi ya Mashujaa waliibuka kidedea zaidi katika mchakato huo, baada ya kujizolea tuzo tano, kupitia mbili za bendi (Wimbo Bora wa Bendi – Risasi Kidole) na Bendi Bora ya Mwaka, huku ikitwaa tatu za wasanii wake, ambao ni Chalz Baba aliyetwaa mbili za Mtunzi Bora wa Mashairi – Bendi na Msanii Bora wa Kiume – Bendi.

Pia nyota wake Fagasoni aliibuka kidedea katika kategori ya Rappa Bora wa Bendi, alikowabwaga Greyson Semsekwa, J4, Jonico Flower na Sauti ya Radi. Ndo kusema Mashujaa wakiongozwa na Chalz Baba, ‘walitisha mno’ usiku ule na kuzipoteza bendi na wanamuziki mahiri wa dansi nchin
Dimpoz na ushindi wa ‘neno bora’ la ‘Usiku wa Tuzo’

Kwangu mimi, msanii Ommy Dimpoz alikuwa zaidi ya mshindi, kwani licha ya tuzo zake tatu, aliibuka mshindi pia kwa kutoa kauli nayoweza kuiita ‘bora zaidi’ kuliko zote zilizotolewa na washiriki wengine zaidi ya 100 waliofika ama kutuma wawakilishi wao.

Nyuma ya ‘neno bora,’ Dimpoz aliitoa tuzo moja kwa Vanessa Mdee, kati ya mbili alizoshinda kupitia kibao alichomshirikisha cha ‘Me and You’ na kutafsiriwa kama ‘aliyempoza’ binti huyo aliyebwagwa katika kategori ya Msanii Bora Anayechipukia, ambayo ilienda kwa Ali Nipishe.

“Napenda kumshukuru kila aliyefanikisha mimi kupata tuzo hii, ambayo nina furaha kwani nimekabidhiwa tuzo hiyo shemeji yangu (akimaanisha Wema Sepetu aliyemkabidhi),” alisema Dimpoz huku akimtania; ‘Kama vipi tukutane baadaye shemeji.’

Akionekana kuiva na semina elekezi kwa wateule ‘nominees’ iliyotolewa na TBL kupitia Bia ya Kilimanjaro, Dimpoz alisema: “Kama msanii na Mtanzania, napenda kusema kuwa, tumechoka kuwazika wasanii maskini wenye majina makubwa katika ‘game.’

“Ifike kipindi kila mmoja kwa nafasi yake aumizwe na hali duni kimaisha na kimapato tuliyonayo wasanii na kuzikwa tukiwa maskini licha ya majina makubwa tuliyonayo na kuyapata katika tasnia hii wakati wa uhai wetu,” alisisitiza Dimpoz huku akiamsha hisia za mashabiki ukumbini.

Ni kauli ambayo haiitaji ufafanuzi, ingawa mwenyewe hakusita kuifafanua: “Serikali na wadau wa muziki nchini, ndio wawezeshaji watakaofanikisha ukubwa wa majina yetu kwenda sambamba na pato letu.

“Serikali itusaidie kupitia michakato sahihi ya hatimiliki na wadau watoe kipaumbele kwa wasanii wa nyumbani. Sio tunafanya tamasha, huku maonesho yetu yakipambwa na picha za kina Messi (Lionel), kama wao ni zaidi yetu, basi waitwe tuone kama watashangiliwa,” alisema.

Dimpoz akawa ametoa ujumbe bora ambao kwangu mimi naupa ushindi wa ‘Neno Bora Zaidi’ la Usiku wa Tuzo, ambalo ni aghalabu kusikia likitamkwa na msanii, badala yake tungetegemea kulipata kutoka kwa Mgeni Rasmi, ambaye KTMA umfanya kuwa ni ‘Brand Manager’ na usiku ule alikuwa ni George Kavishe, Meneja wa Bia ya Safari.

Hussein Jumbe, Zahir Ali ‘Zorro’ Jose Mara wafunika

Burudani ukumbini zilianza saa 3:30 usiku kwa Mrisho Mpoto na wakali wanaounda Mjomba Bendi, waliopanda jukwaani baada ya dakika moja ya maombolezo ya kifo cha Ngwea – ambaye picha za msanii zilioneshwa katika kila ‘screen’ iliyokuwa ukumbini hapo.

Ahadi ya burudani kali kwa watakaohudhuria ‘Usiku wa Tuzo’ iliyotolewa na Kavishe ikaanza kudhihiri wasanii waliotumbuiza walipokuwa jukwaani. Amini Mwinyimkuu ‘Amini’ alifuata ‘Kikwetu Kwetu’ akiuchanganya wimbo wake wa Ni Wewe na ngoma ya Kabila la Wamakonde ‘Sindimba.’

Mtangazaji na Mtayarishaji wa Kipindi cha Supa Mix cha East African Radio na Uswazi cha East African TV, Hillary Daudi ‘Zembwela,’ akafuata mara kadhaa jukwaani na visa vilivyovunja mbavu vya Bure Mbaya kilichohusisha Dereva wa gari ya vichaa na kile cha Busara Haiuzwi kilichohusisha muuza mahindi mwenye kigugumizi.

Licha ya Zembwela kufunika na simulizi ya visa hivyo na vingine kibao, bado mashabiki hawatowasahau wakali wa muziki nchini Hussein Jumbe na Zahir Ali ‘Zorro,’ waliowapagawisha kwa aina ya muziki usio wao na nyimbo zisizokuwa zao pia huku wakizitendea haki.

Zilikuwa dakika 10 za kukata na shoka, ambapo Jumbe aliingia ukumbini saa 5:32 na kibao cha Zeze kilichoimbwa na Khaleed Mohammed TID. Zeze la Jumbe likaacha gumzo ukumbini, huku nyota huyo wa dansi akikitendea haki stejini kwa kukicheza na kunata na mistari.

Katika staili ya bandika-bandua ‘non-stop,’ saa 5:37, Jumbe akampisha Zorro aliyepanda na kibao cha Kikulacho kinguoni mwako, kilichoimbwa na mkali wa TAKEU, Lucas Mkenda ‘Mr Nice.’ Manjonjo ya Zorro wakawakumbusha wengi zama za Mr Nice. Hakika Zorro na Jumbe wakaacha midomo wazi mashabiki.

Mfululizo huo wa burudani za bandika bandua, ukaendelea saa 6:22, ambapo Barnabas Elias ‘Barnaba’ na Snura ‘Mama Majanga’ walifululiza kwa burudani kali, kisha kupisha tuzo kadhaa, kabla ya saa 6:55 mizuka ya wengi ukumbini kupandishwa tena na Jose Mara.

Jose mmoja wa nyota wanaounda kundi la Mapache Watatu, alijikusanyia fedha nyingi zaidi za kutuzwa jukwaani, ‘alipowakimbiza’ mashabiki kupitia kibao cha ‘Kinyaunyau’ cha Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje,’ na kufanya mfuko wa shati lake la Kinigeria kujaa noti na nyingine kumwagwa chini.

Lady Jaydee, Diamond wazua manung’uniko

Kama inavyoaminika, hakuna zuri lisilo na kasoro; Usiku wa Tuzo pia ulithibitisha kauli hii ya wahenga, ambapo baadhi ya mashabiki nje ya ukumbi katika ‘Red Carpet’ na hata ukumbini walionekana kukwazwa na kukosekana kwa wakali kadhaa wa muziki wakiwamo Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Judith Wambura ‘Lady Jaydee.’

Diamond Platnumz, aliyeibuka mshindi wa medali mbili za Msanii Bora wa Kiume na ile ya Msanii Bora wa Kiume wa Bongo Flava, haikuelezwa nini kilisababisha kutofika ukumbini, ambapo tuzo zake hizo zilipokelewa kwa niaba yake na binti ambaye hata hivyo hakujitambulisha ni nani.

Hamu ya mashabiki kumuona Diamond iliyoanzia katika ‘Red Carpet’ ikaamshwa upya kila alipotajwa kushinda tuzo na kuzua maswali miongoni mwa mashabiki wake, kama ilivyokuwa pia kwa ‘swahiba’ wake wa siku za karibuni, Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Ney wa Mitego.

Ilikuwa hivyo kwa Jaydee. Mrembo wa Tanzania 2012, Brigite Alfred ndiye aliyepanda jukwaani kumtangaza mshindi wa kategori ya Msanii Bora wa Kike, ambapo Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti Almasi na Recho walikuwa wakichuana.

Brigite akashika karatasi yenye jina la mshindi aliyoitoa katika bahasha na aliposema: Mshindi wa Msanii Bora wa Kike niii…..mashabiki wakalipuka kwa kelele ukumbini na kumalizia Lady Jaydeeeeeee!!!! Na wakarudia jina hilo mara kadhaa, kuionesha kukosa kwake mpinzani.

Ndipo aliposoma kwa kutaja jina la Jaydee kuwa mshindi na kuamsha shangwe ukumbini, iliyokuja kusindikizwa na maneno; shemejiii, shemejiiii, kufuatia mume wa Jaydee, Gadna G. Habashi kupanda jukwaani kumpokelea tuzo hiyo ya kategori pekee kwa nyota huyo mwaka huu.

Licha ya utetezi wa Gadna kuwa Jaydee yu safarini mkoani Shinyanga alikoenda kutumbuiza katika kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo wa mkoa huo, bado kiu ya mashabiki hao haikuweza kukatwa.

Ndipo Gadna alipowaamsha upya mashabiki hao alipowapa ujumbe wa nyota huyo wa kuwakaribisha katika tamasha la Juni 14 la kuadhimisha Miaka 13 ya Jaydee katika muziki, litakalofanyika kwenye Ukumbi wake wa Nyumbani Lounge, ambapo waliitikia: Tutakujaaaaaaaaa!!!!

Kauli ya mama wa Sharo Milionea/Ahadi za washindi

Kama ilivyotarajiwa, washindi wa tuzo mbalimbali walikuwa na kauli tofauti, zilizotanguliwa na ile ya Mama wa aliyekuwa mkali wa maigizo na muziki wa Bongo Flava, Ramadhani Mkieti ‘Sharo Milionea,’ Zaina Mkieti, aliyekuwa ndani ya Ukumbi wa Mlimani City kumwakilisha mwanaye aliyekuwa akiwania tuzo mbili.


Sharo Milionea alikuwa akiwania tuzo za Wimbo Bora wa Bongo Pop na Wimbo Bora wa Kushirikiana kupitia Chuki ni Bure aliomshirikisha Dully Sykess na akiwa katika ‘Red Carpet,’ Zaina akafunguka kuhusu tuzo hizo na namna anavyojisikia miezi sita tangu kifo cha mwanaye.

“Nashukuru kwa yote, michakato iliyofanikisha mimi kuwa hapa leo, lakini pia mwanangu kuwa mteule ‘nominees’ bila kujali kama atashinda ama atashindwa. Miezi sita sasa tangu kufariki kwa mwanangu, tukio hili linanipa faraja kuona kuwa Watanzania bado wanathamini kazi za marehemu mwanangu,” alisema Zaina.

Pia mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Citizen cha nchini Uganda (ambaye jina lake halikupatikana), aliyepokea tuzo Jose Chameleon, aliyeshinda kategori ya Wimbo Bora wa Afrika Mashariki, kupitia kibao cha Valu Valu, alikuwa na machache kuhusu muziki Afrika Mashariki.

Mtangazaji huyo alitoa ujumbe wa Chameleon kwa Watanzania, akiwataka wasanii na mashabiki wake kutoachwa nyuma na michakato mbalimbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, badala yake wajiunge ili kupaa pamoja kimuziki nje ya ukanda huo unaojumuisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.

“Ahsante Mungu kwa kunipa tuzo nyingine, ingawa hii nayo haitokani na wimbo mwingine, nakuomba wewe unijalie kazi nyingine, itakayoweza kutisha na kutwaa tuzo za mwaka mwingine,” alishukuru na kuahidi Kala Jeremiah akiigizia kibao chake cha Dear God kilichompa tuzo zake.

Jeremiah akaamsha simanzi ukumbini kwa kauli hii: “Katika Dear God, nilikuwa na maombi maalum kwa waliokuwa wagonjwa wetu; Sadick Juma Kilowoko (Sajuki) na Fatma Bint Baraka ‘Bi Kidude.’ Niliwaombea kwa Mungu kuonesha navyowapenda, lakini Mungu kawapenda zaidi.”

Jeremiah akawataka Watanzania kupendana kila mmoja kwa nafasi yake, ambapo yeye atawaenzi Sajuki na Bi Kidude aliowaombea katika wimbo huo, pamoja na ‘msela wake’ Ngwea kwa kuhakikisha anafanya kilicho bora kila mwaka. Akamaliza kwa kumtakia uponaji mwema na wa haraka, Rita Poulsen ‘Madam Rita.’

“Amenitoa mbali Madam na alipaswa kuwa hapa kushuhudia matunda haya pamoja na kupokea moja ya tuzo hizi, lakini kutokana na tukio la ajali lililompata, hayuko ukumbini hapa na sisi, namuombea kwa ‘Dear God’ apone haraka,” alisema Jeremiah na kushangiliwa na mashabiki.

Msanii Chalz Baba, aliahidi kuwalipa mashabiki waliompigia kura yeye na bendi yake ya Mashujaa kwa kuwadondoshea ‘kibao’ kipya cha ‘Ushamba Mzigo,’ huku Luiza Mbutu aliyeshinda tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Bendi, ‘akii-dedicate’ tuzo hiyo kwa mashabiki wa Twanga Pepeta.

Washindi wa tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka wa Raggae, kundi la Warriors From The East, wakatoa shukrani za dhati kwa waasisi wa muziki huo nchini Innocent Garinoma, Innocent Nganyagwa ‘Ras Inno’ na wengineo kwa harakati zilizoifikisha reggae mahali ilipo sasa.

Fred Maliki ‘Mkoloni’ aliyepanda jukwaani kupokea tuzo ya Wimbo Bora wa wa RnB kwa niaba ya Rama Dee aliyeshinda kupitia kibao Kuwa na Subira alichowashirikisha Mapacha, alisema nyakati za ‘vinega kuwa busy’ kikazi unaendelea kutokana na vita dhidi ya wanyonyaji kushika kasi

No comments:

Post a Comment